Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amekubali kuchukua mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo, hatua itakayoendeleza muda ambao amekaa katika klabu hiyo.
Mfaransa huyo amekuwa meneja wa Arsenal kwa miaka 21 sasa.
Wenger na mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke walikutana Jumatatu kuamua hatima ya meneja huyo, na kisha uamuzi wao ukawasilishwa kwa mkutano wa bodi Jumanne.
Arsenal wanapanga kutangaza rasmi uamuzi huo Jumatano.
Gunners walimaliza Ligi ya Premia wakwia nafasi ya tano, mara yao ya kwanza kumaliza chini ya nafasi ya nne tangu Wenger alipojiunga nao mwaka 1996.
Walimaliza alama 18 nyuma ya mabingwa Chelsea, lakini walifanikiwa kuwachapa Blues katika fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley Jumamosi.
Mkataba wa Wenger ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.